Mgogoro wa hali mbaya ya usalama wa chakula washtadi Kongo DR
Kuongezeka mapigano na mgogoro wa kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumezidisha tatizo la uhaba wa chakula nchini humo.
Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa matabaka mbalimbali ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo khususan katika mji mkuu Kinshasa hivi sasa wanajidhaminia milo yao ya siku kwa wauzaji wa vibanda vya mitaani vinavyouza chakula kwa bei ya chini (Malewa); vibanda ambavyo vimetajwa kuwa havikidhi viwango vya usafi na kanuni za afya. Familia mbalimbali za Wakongo zimelazimika kujikidhia mahitaji yao ya chakula katika vibanda hivyo kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Viongozi wa sekta ya afya na tiba wa Kongo kwa upande wao wanaamini kuwa manunuzi ya vyakula hivyo vya bei ya chini na visivyokidhi viwango vya kanuni za afya yamesababisha hivi sasa kuongezeka kwa kiasi kikubwa magonjwa ya kuambukiza na ya hatari ikilinganishwa na miaka iliyopita. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa nchi maskini ya katikati mwa Afrika licha ya nchi hiyo kuwa na maliasili tajiri yakiwemo madini mbalimbali. Hatua ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo ya kukataa kuondoka madarakani licha kumalizika muda wa wake wa urais mwezi Disemba uliopita imeifanya hali ya kisiasa nchini humo kuwa mbaya. Baadhi ya raia wa Kongo DR waliohojiwa wamesema kuwa kuzidi kuwa mbaya hali ya maisha ndio sababu inayowafanya wananchi wale chakula wanachoweza kujigharamia.