Uchaguzi wa Rais na Bunge Libya kufanyika kabla ya Februari 2018
Uchaguzi wa Rais na Bunge wa Libya umepangwa kufanyika kufikia mwezi Februari mwaka kesho.
Pande zinazozozana huko Libya ambazo zimejielekeza huko Misri kwa ajili ya mazungumzo na mashauriano ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo zimekubaliana kuhusu kufanyika chaguzi hizo kabla ya Februari mwaka kesho. Duru za habari za Misri zimearifu kuwa mazungumzo yaliyofanywa na pande hasimu huko Libya yamepelekea kufikiwa muafaka wa kuunda kamati ya pamoja yenye wawakilishi 30 wa bunge na wa baraza kuu la nchi hiyo; na kwamba kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza masuala yote yaliyofikiwa na pande hizo kuhusu marekebisho yanayopasa kufanyika huko Libya.
Aidha bunge la wawakilishi la Libya litaifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo na hivyo kuweza kufikiwa muafaka wa kisiasa. Kulinda umoja wa ardhi yote, kuendeleza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na magenge ya magendo ya binadamu na vile vile kuendelea kuwasili wimbi la wahajiri haramu kupitia nchi hiyo wanaotoka katika nchi mbalimbali za Kiafrika kwa lengo la kuelekea barani Ulaya, kupungua uzalishaji wa mafuta na bei yake katika masoko ya kimataifa, ni miongoni mwa matatizo yanayoisumbua Libya hivi sasa.