Njaa yatishia mamia ya maelfu ya watu nchini Somalia
Mwakilishi maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametahadharisha kuhusu tishio kubwa la njaa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na ametoa wito wa kuchukua hatua haraka ili kuzuia maafa ya kibinadamu.
Kay Nicholas, mwanadiplomasia wa Uingereza ambaye hadi hivi karibuni alikuwa akihudumu kama mjumbe wa Umoja wa Mataifa huko Somalia amesema kuwa mamia ya maelfu ya watu nchini humo wanaweza kuaga dunia mwezi Mei mwaka huu iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kuondoa tishio hilo la njaa lililoiathiri Somalia.
Wakati huo huo Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa fedha zinahitajika ili kutoa misaada kwa raia milioni 3.9 huko Somalia, na wakati huo huo fedha zaidi zinahitajika ili kuweza kukabiliana na hali ya mambo inayozidi kuwa mbaya siku baada ya siku.
Ofisi hiyo imeongeza kuwa watu milioni tano wanahitaji msaada huko Somalia. Umoja wa Mataifa umeomba msaada wa kibinadamu wa dola milioni 864 kwa ajili ya kukabiliana na baa la njaa huko Somalia mwaka huu.