Mwanaharakati Zimbabwe asema atachuana na Mugabe uchaguzi wa 2018
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25348-mwanaharakati_zimbabwe_asema_atachuana_na_mugabe_uchaguzi_wa_2018
Kiongozi wa harakati ya malalamiko ya wananchi nchini Zimbabwe ametangaza kuwa atagombea kiti cha rais dhidi ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2017 04:16 UTC
  • Mwanaharakati Zimbabwe asema atachuana na Mugabe uchaguzi wa 2018

Kiongozi wa harakati ya malalamiko ya wananchi nchini Zimbabwe ametangaza kuwa atagombea kiti cha rais dhidi ya Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwakani.

Mchungaji Evan Mawarire aliyasema hayo nje ya mahakama mjini Harare ambapo kesi dhidi yake inatazamiwa kusikilizwa mwezi ujao wa Machi. Mwanaharakati huyo anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia na kuhatarisha usalama wa taifa, kwa kuandaa maandamano bila kibali cha serikali. 

Mwaka uliopita, kiongozi huyo wa kidini alianzisha kampeni katika mitandao ya kijamii chini ya kaulimbiu 'Harakati ya Hii Benera' ambapo maelfu ya wananchi walijitokeza na kufanya maandamano dhidi ya serikali. 

Maandamano ya wananchi dhidi ya serikali

Harakati hiyo inayoongozwa na Pastor Mawarire inahesabiwa kuwa kubwa zaidi dhidi ya serikali ya Rais Mugabe katika miaka ya hivi karibuni, na tayari Morgan Tsvangirai, mkuu wa chama cha upinzani cha Movemenf for Democratic Change (MDC)  ametangaza kuiunga mkono.

Licha ya ukongwe na tetesi kuhusu hali yake ya kiafya, Mugabe mwenye umri wa miaka 99 na ambaye amekuwa madarakani nchini Zimbabwe tangu mwaka 1980, amesema yupo tayari kutetea kiti chake katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 2018. Siku chache zilizopita, mkewe alisema "Zimbabwe itampigia kura Mugabe hata akiwa maiti".

Rais Mugabe na mkewe Grace