UN: Kesi ya mtoto wa rais wa zamani wa Libya ipelekwe ICC
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kupelekwa faili la kesi ya Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa Libya katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hukumu ya kifo dhidi ya Saif al-Islam aliyotolewa Julai mwaka 2015 pasina yeye kuwepo mahakama ni kejeli kwa mchakato wa haki na sheria.
Amesema mchakato wa kesi hiyo siyo tu ilikiuka sheria za Libya, bali pia ulikosa kufikia viwango vya kimataifa haswa kwa kutilia maanani kuwa mtoto huyo wa Gaddafi alikuwa anaandamwa na mashtaka ya mauaji na jinai nyingine dhidi ya binadamu.
Mwaka jana kulienea ripoti katika mitandao ya habari juu ya uwezekano wa kuachiliwa huru Saif al-Islam Gaddafi, huku vyombo vingine vya habari vikitilia shaka endapo mwana huyo wa Muammar Gaddafi bado yuko jela nchini Libya au la.
Hata hivyo serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ilikanusha madai hayo na kusema kuwa, matamshi ya Al-Ajmi Al-Atiri, kamanda wa jela ya Zintan anakozuiliwa Saif al-Islam, ya kutaka kuonyesha kuwa kuna uwezekano wa kutoadhibiwa mwana huyo wa kiume wa Gaddafi na watuhumiwa wengine wa uhalifu na jinai za kibinadamu, hayakubaliki.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na watu hao haziwezi kusamehewa hata baada ya kupita muda mrefu.