20 wauawa katika machafuko katikati mwa Mali
-
Askari wa kulinda amani wa kimataifa nchini Mali
Serikali ya Mali imetangaza habari ya kuuawa watu 20 katika machafuko ya kikabila yaliyoyakumba maeneo ya katikati mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Wizara ya Masuala ya Usalama wa Nchi ya Mali imetangaza habari hiyo leo Jumapili na kuongeza kuwa, machafuko hayo yaliyotokea wiki iliyopita kwenye maeneo ya Kama na Sènèbamanan katikati mwa Mali, yamewahusisha wafuasi wa kabila la Fulani na lile la Wabambara na kupelekea watu wasioupungua 20 kuuawa na wengine 16 kujeruhiwa.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, machafuko hayo yamewasababishia hasara za vitu na mali, watu wasiopungua 600.
Watu 24 wametiwa mbaroni wakihusishwa na machafuko hayo. Machafuko yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini Mali tangu mwaka 2012 wakati yalipotokea mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Serikali na makundi ya watu wenye silaha yalifikia makubaliano ya amani mwaka 2015 kwa lengo la kudumisha utulivu katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi hiyo. Hata hivyo machafuko na mauaji yanaendelea kuripotiwa kwenye maeneo hayo.
Askari wa Umoja wa Mataifa pamoja na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini Mali mwaka 2013 lakini nao wameshindwa kuleta utulivu na kukomesha mapigano nchini humo.