Sisitizo la kuundwa kamati maalumu ya kusimamia makubaliano ya Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25706-sisitizo_la_kuundwa_kamati_maalumu_ya_kusimamia_makubaliano_ya_kongo
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa kuna udharura wa kuundwa kamati maalumu ya kusimamia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya serikali na vyama vya upinzani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2017 10:39 UTC
  • Sisitizo la kuundwa kamati maalumu ya kusimamia makubaliano ya Kongo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa kuna udharura wa kuundwa kamati maalumu ya kusimamia makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya serikali na vyama vya upinzani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  limevitolea wito vyama mbalimbali huko Kongo kuzidisha juhudi ili kuharakisha mchakato wa mazungumzo na hivyo kuweza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na upinzani tarehe 31 Disemba mwaka jana. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limetaka kuteuliwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo na kuundwa kamati ya kusimamia makubaliano hayo. 

Mpatanishi wa Kanisa Katoliki Kongo Askofu Marcel Utembi akiwasili na wawakilishi wengine katika mazungumzo ya Kongo siku moja kabla ya kufikiwa makubaliano

Aidha limesisitiza kuwa linaunga mkono makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya serikali na wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu namna ya kuiendesha nchi hadi pale uchaguzi mkuu utakapofanyika. Licha ya kwamba serikali na wapinzani huko Kongo hivi sasa wanajaribu kufikia muafaka kuhusu namna watakavyotekeleza makubaliano hayo, lakini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi wake kuhusu kutopiga hatua mazungumzo yanayohusiana na utekelezaji wa makubaliano hayo. Kwa mujibu wa makubaliano  ya awali yaliyofikiwa kati ya serikali ya Kongo na wapinzani tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana, Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo ataendelea kuwepo madarakani hadi Disemba mwaka huu hadi kutakapofanyika chaguzi za Rais na Bunge, licha ya kumalizika muhula wake wa urais mwaka uliopita.