IGAD yaitisha mkutano maalumu kuhusu wakimbizi wa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25758-igad_yaitisha_mkutano_maalumu_kuhusu_wakimbizi_wa_somalia
Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD imeitisha mkutano maalumu mjini Nairobi Machi 25, ili kujadili suluhisho la kudumu la wakimbizi wa Somalia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 28, 2017 12:52 UTC
  • IGAD yaitisha mkutano maalumu kuhusu wakimbizi wa Somalia

Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD imeitisha mkutano maalumu mjini Nairobi Machi 25, ili kujadili suluhisho la kudumu la wakimbizi wa Somalia.

Jumuiya hiyo inayoundwa na nchi za Kenya, Uganda, Somalia, Djibouti, Sudan, Ethiopia, Eritrea na Sudan Kusini imesema mkutano huo utahimiza kutumiwa fursa zilizopatikana hivi karibuni katika ngazi ya taifa, kikanda na duniani kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Somalia.

Uamuzi wa kuitishwa mkutano huo maalumu ulichukuliwa katika mkutano wa kawaida wa IGAD uliokutanisha wakuu wa nchi na serikali ambao ulifanyika Septemba 13, 2016, Mogadishu nchini Somalia. Mkutano huo pia utahimiza kuendelea kupewa hifadhi na kulindwa wakimbizi kutoka Somalia na pia mpango wa kuwawezesha wakimbii kujitegemea sambamba na kuzisaidia jamii zinazowapokea wakimbizi. Aidha kikao hicho cha IGAD kitajadili namna ya kuwarejesha nyumbani kwa hiari wakimbizi Wasomali.

Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Kenya ilisema kuwa uamuzi wa serikali ya Kenya wa kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab sio wa kisheria.

Akitoa hukumu yake kuhusiana na suala hilo, Jaji John Mativo wa Mahakama Kuu ya Kenya alisema kwamba hatua ya serikali ya Nairobi ya kutaka kufunga kambi hiyo ilitokana na utumizi mbaya wa madaraka na ubaguzi ambao unapingana na katiba ya nchi hiyo pamoja na sheria za kimataifa. Uamuzi huo wa serikali ulikosolewa pakubwa na mashirika ya kimataifa.

Zaidi ya Wasomali milioni 2 wamekimbia makazi yao kutokana na mgogoro mkubwa ambao sasa umeingia katika muongo wa tatu.