Ripoti: Maelfu ya raia wamekuwa wakimbizi kaskazini mashariki mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25830-ripoti_maelfu_ya_raia_wamekuwa_wakimbizi_kaskazini_mashariki_mwa_nigeria
Maelfu ya raia katika vijiji vya kaskazini mashariki mwa Nigeria wamelazimika kuwa wakimbizi wakihofia hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Mar 02, 2017 07:49 UTC
  • Ripoti: Maelfu ya raia wamekuwa wakimbizi kaskazini mashariki mwa Nigeria

Maelfu ya raia katika vijiji vya kaskazini mashariki mwa Nigeria wamelazimika kuwa wakimbizi wakihofia hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na duru za kieneo za Nigeria zimetangaza kuwa, karibu watu elfu saba ambao ni wakazi wa vijiji vya eneo la msitu wa Sambisa ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria wameyakimbia makazi yao.

Ripoti zinaeleza kuwa, katika majuma ya hivi karibuni idadi ya raia wanaoyakimbia makazi yao katika eneo hilo imeongezeka kutokana hofu ya hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wanachama wa Boko Haram

Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Nigeria imekuwa ikidai katika ripoti zake za hivi karibuni kwamba, jeshi la nchi hiyo limepata mafanikio makubwa katika vita vyake dhidi ya wapiganaji wa kundi la kitakfiri la Boko Haram. Katika upande mwingine ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, asilimia 65 ya wakazi wa jimbo la Borno huko kaskazini mwa Nigeria ambako ndiko yaliko makao makuu ya Boko Haram wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa. 

Kundi la Boko Haram lilianzisha harakati zake za uasi mwaka 2009 nchini Nigeria na kupanua wigo wa hujuma zake mwaka 2015 katika nchi jirani na Nigeria za Niger, Chad na Cameroon. Zaidi ya watu 20,000 wameuawa kutokana na hujuma na mashambulio ya kundi hilo huku wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita wakibaki bila ya makazi.