Jeshi la Kenya: Tumewaangamiza makumi ya wanachama wa genge la ash-Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25856-jeshi_la_kenya_tumewaangamiza_makumi_ya_wanachama_wa_genge_la_ash_shabab
Msemaji wa Jeshi la Kenya amesema kuwa, askari wa nchi hiyo wamewaangamiza wanachama 57 wa genge la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab, kusini mwa Somalia katika operesheni pana iliyofanywa dhidi ya magaidi wa kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2017 00:38 UTC
  • Jeshi la Kenya: Tumewaangamiza makumi ya wanachama wa genge la ash-Shabab

Msemaji wa Jeshi la Kenya amesema kuwa, askari wa nchi hiyo wamewaangamiza wanachama 57 wa genge la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab, kusini mwa Somalia katika operesheni pana iliyofanywa dhidi ya magaidi wa kundi hilo.

Jenerali Joseph Owuoth amesema kuwa jeshi la Kenya chini ya mwamvuli wa kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, kwa kutumia makombora na helikopta za kivita lilishambulia ngome za wanachama wa kundi hilo la kigaidi katika mji wa Afmadow, kusini mwa Somalia ambapo kwa akali mahaidi 57 waliuawa. Mji wa Afmadow unajulikana kwa kuwa na ngome nyingi za kundi la ash-Shabab.

Askari wa KDF 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mashambulizi hayo ya jeshi la Kenya, magari kadhaa na silaha za wanachama wa kundi hilo yaliteketezwa. Kabla ya hapo duru za habari ziliripoti kwamba jeshi la Kenya kwa kushirikiana na serikali ya Mogadishu, lilipeleka askari wake kutoka maeneo ya mpakani kwenda maeneo ya kusini mwa Somalia. Lengo la hatua hiyo ya jeshi la Kenya ni kupata uzoefu zaidi na kuwaondoa wapiganaji wa ash-Shabab kutoka maeneo ya mpakani ya Somalia na Kenya.

Wanachama wa ash-Shabab waliouawa

Hii ni katika hali ambayo genge hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah, limetoa vitisho vikali dhidi ya serikali mpya ya Somalia. Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika, waliwafurusha wanachama wa kundi hilo kutoka Mogadishu, mji mkuu wa Somalia hapo mwaka 2011 ingawa hadi sasa baadhi ya maeneo ya mji huo bado yako mikononi mwa magaidi hao.