Wafadhili waahidi kuunga mkono Somalia
Wafadhili wa kimataifa wameahidi kuendelea kuunga mkono Kikosi cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM, ili kiweze kufikia lengo lake kuu la kurejesha uthabiti Somalia.
Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa, Uingereza na Kituo cha Afrika cha Utatuzi Bora wa Migogoro wametoa taarifa ya pamoja na kuahidi kusaidia kurejesha amani Somalia.
Walitoa ahadi hiyo baada ya kumalizika mkutano wa siku tano mjini Nairobi siku ya Alhamisi, mkutano ambao ulihudhuriwa na uongozi wa ngazi za juu wa AMISOM. Mkutano huo uliitishwa kutayarisha bajeti ya AMISOM ambayo pia itajumuisha stratejia ya kikosi hicho kuondoka Somalia katikati ya mwaka 2018.
Wakati huo huo mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM Francisco Madeira amesema atashirikiana kwa karibu na waziri mkuu mpya wa Somalia Bw. Hassan Ali Khaire ili kutuliza hali ya nchi hiyo.

Madeira amesema ana imani na Khaire ambaye aliapishwa kuwa waziri mkuu na kuahidi kuimarisha usalama na kupambana na ufisadi na kuongeza kuwa uzoefu wa Khaire katika kazi za kibinadamu na biashara utakuwa muhimu kwa serikali mpya.
AMISOM inajumuisha wanajeshi 22,000 kutoka Kenya, Burundi, Djibouti, Ethiopia na Uganda ambao walianza sughuli za kurejesha amani Somalia mwaka 2007.