Hali ya hatari yatangazwa mpaka wa Mali na Niger
(last modified Sat, 04 Mar 2017 16:08:57 GMT )
Mar 04, 2017 16:08 UTC
  • Hali ya hatari yatangazwa mpaka wa Mali na Niger

Serikali ya Niger imetangaza hali ya hatari katika mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani ya Mali.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Niger imesema kuwa, hali hiyo ya hatari imetangazwa katika maeneo ya mpaka wa nchi hizo mbili kwa shabaha ya kupunguza idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi hususan katika maeneo ya Tillabéri na Tahoua. 

Hali hiyo itaruhusu kupelekwa askari zaidi katika maeneo ya mpaka wa pamoja wa Mali na Niger na kuruhusu jeshi kukagua maeneo na makazi ya raia wa magharibi mwa Niger. 

Taarifa ya serikali ya Niger imesema hali ya maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Mali si shwari kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika katika maeneo hayo.

Askari wa jeshi la Niger wakifanya doria

Askari 16 wa serikali ya Niger waliuawa katika shambulizi lililofanyika siku kadhaa zilizopita katika maeneo hayo na wengine 18 wameheruhiwa.

Niger inakabiliwa na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na hujuma zinazofanywa mara kwa mara na makundi yenye mitazamo ya kufurutu mipaka katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Mali.  

Tags