Jeshi la Nigeria laendelea na oparesheni ya kuwaangamiza Boko Haram
Jeshi la Nigeria limesema kuwa linaendelea na oparesheni ya kuwaangamiza wanamgambo wa Boko Haram katika maficho yao.
Kanali Sani Kukasheka, Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa vikosi vya jeshi hilo vimefanikiwa kuyasafisha kikamilifu maeneo mawili ya Dure yanayopatikana katika jimbo la Borno kwa kuwaangamiza wanamgambo wa Boko Haram waliokuweko katika maeneo hayo.
Kanali Kukasheka ameongeza kuwa wanajeshi zaidi ya 150 wameongezwa ili kusaidia utekelezaji wa oparesheni hiyo dhidi ya maficho ya Boko Haram katika maeneo hayo mawili ya Dure moja na mbili.
Maeneo hayo mawili ya Dure moja na Dure mbili yako katika msitu wa Sambisa ambao umekuwa ni maficho ya utoaji mafunzo na ngome kubwa ya wanamgambo wa Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa wamenasa silaha kadhaa, magari, pikipiki na vyakula katika oparesheni dhidi ya ngome ya Boko Haram.