Maafisa wawili wa UN watekwa nyara Kongo DR
Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden wametekwa nyara katika mkoa wa Kasai katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Maafisa wa serikali ya Kongo wamewataja maafisa hao wa UN kuwa ni Michael Sharp wa Marekani na Zahida Katalan wa Sweden. Wamesema kuwa hadi kufikia sasa bado hawajawatambua watu waliowateka nyara maafisa hao. Sharp na Katalan walikuwa miongoni mwa wataalamu wa timu ya Umoja wa Mataifa inayochunguza mizozo iliyoiathiri Kongo tangu katikati ya muongo wa 90, wakati vita vya ndani vilipoibua makumi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha na kupelekea kuingia nchini humo majeshi ya nchi sita jirani.
Lambert Mende msemaji wa serikali ya Kongo ameeleza kuwa, wataalamu hao wa timu ya Umoja wa Mataifa walitekwa nyara katika daraja moja katika mto Moyo na kupelekwa msituni na wavamizi wasiofahamika. Charles-Antoine Bambara msemaji wa kikosi cha kudumisha Amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) amesema kuwa maafisa hao wawili wa umoja huo walitoweka tangu juzi Jumapili. Maafisa wa Kongo na wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa juhudi za kuwapata maafisa hao zinaendelea.