Amnesty yailaumu serikali kwa maporomoko ya taka Ethiopia, waliokufa wakifikia 65
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema serikali ya Ethiopia inabeba dhima ya vifo vya makumi ya watu katika mkasa wa maporomoko ya udongo katika eneo la kutupa taka viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa.
Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International eneo la Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu amesema kuwa, serikali ya Ethiopia inafaa kulaumiwa kwa kushindwa kuzuia mkasa huo ambao ungeweza kuzuilika.
Amesema: "Licha ya serikali kufahamu fika kuwa sehemu hiyo ya kutupa taka imejaa hadi pomoni na ni hatari kwa afya na maisha ya binadamu, lakini ilishindwa kuchukua hatua yoyote kuepusha maafa hayo."
Afisa huyo wa Shirika la Msamaha Duniani amesisitiza kuwa, serikali haina budi kufanya juu chini kuhakikisha kuwa imejua hatima ya makumi ya wahanga wa mkasa huo wa Jumamosi, na manusura wanapewa makaazi mbadala na hali zao za kiafya zinashughulikiwa.
Inaarifiwa kuwa, zaidi ya watu 150 walikuwa wanaishi katika nyumba za mabanda katika eneo hilo linalofahamika kama Koshe (taka), na wamekuwa wakilichakura jalala hilo ili kupata angalau kitu cha kula au vitu vya kuuza kama plastiki ili kujikimu kimaisha.
Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo imeongezeka na kufikia watu 65, kutoka 48 iliyoripotiwa awali. Mkasa huo ulitokea baada ya makumi ya watu kufukiwa na maporomoko ya udongo katika eneo kubwa la kutupa taka, viungani mwa mji mkuu Addis Ababa Jumamosi iliyopita.