Kuundwa kundi shirikishi kwa ajili ya kupambana na wahajiri haramu
Serikali za Uhispania, Ufaransa na Niger zimeunda muungano wa pamoja kwa ajili ya kupambana ipasavyo na kadhia ya wahajiri haramu na magendo ya binaadamu.
Juan Ignacio Zoido, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Uhispania ambaye alikuwa amesafiri nchini Niger pamoja na Bruno Le Roux Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, amesema kuwa, Uhispania na Ufaransa zimeunda kundi hilo la pamoja ndani ya nchi hiyo ya Kiafrika ambalo litakuwa na jukumu la kufanya uchunguzi katika kupambana na uhajiri haramu na magendo ya binaadamu.
Katika safari hiyo ya Niger, mawaziri hao wa nchi za Ulaya, kwa kushirikiana na maafisa wa polisi wa Uhispania na Niger walitia saini makubaliano ya ushirikiano katika uga huo. Ni muda sasa ambapo wimbi la uhajiri haramu kuelekea barani Ulaya, limegeuka kuwa tatizo kubwa lisiloweza kutatuliwa na nchi za eneo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, nchi hizo zilijitahidi sana kuchukua hatua kali na kutekeleza sera ngumu kwa ajili ya kuwazuia wahajiri haramu kuelekea barani Ulaya. Sera hizo zilipelekea kubadilika mkondo wa njia za kuelekea barani humo ikiwemo utumiaji wa bahari ya Mediterania.
Itakumbukwa kuwa, akthari ya nchi nyingi za Kiafrika zilikuwa makoloni ya nchi za Magharibi, hususan Ufaransa; na kutokana na hilo mataifa hayo yamekuwa yakifanya juhudi zaidi kwa lengo la kupenyeza tena ushawishi wao ndani ya nchi za eneo. Hata kama harakati za wananchi ziliweza kufanikisha nchi zao kujinasua kwenye makucha ya ukoloni, lakini hadi sasa mataifa hayo ya kikoloni bado yanaendelea kuingilia masuala ya ndani ya makoloni yake ya zamani kupitia ukoloni mamboleo. Kuzusha hitilafu na mapigano ya ndani katika nchi hizo, kuunga mkono kwa siri kwa makundi ya wanamgambo na kupeleka askari wao kupitia fremu ya kuimarisha usalama na uthabiti katika eneo, ni miongoni mwa siasa za kileo za nchi makoloni dhidi ya mataifa ya Kiafrika.
Katika miaka ya hivi karibuni na kwa kutumia visingizio tofauti,Ufaransa na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya zimetuma askari wao katika nchi nyingi za Kiafrika. Hata hivyo si tu kwamba nchi hizo hazikuchukua hatua yoyote ya maana katika fremu ya ushirikiano wa kuleta ustawi na kuboresha hali ya uchumi ya nchi hizo za Kiafrika, bali zimehusika pia kuzirejesha nyuma makusudi nchi hizo kimaendeleo katika fremu ya kulinda maslahi yao binafsi. Hii ni kusema kuwa hadi sasa nchi nyingi za Kiafrika zingali zinakabiliwa na matatizo chungu nzima ya kiuchumi, umasikini uliokithiri na ukosefu wa ajira, huku moto wa vita na mapigano ukiendelea kutokota katika maeneo mengi ya bara hilo na hivyo kuvuruga usalama na uthabiti.
Wimbi la uhajiri hususan la vijana kuelekea nchi za Ulaya, nalo limeendelea kuongezeka siku hadi siku. Uhajiri huo aghlabu hufanyika kupitia njia hatarishi na bahari ya Mediterania. Hii ni katika hali ambayo mazingira ya kisiasa ya nchi kama vile Libya, licha ya kurahisisha suala la wahajiri wa Kiafrika kwenda barani Ulaya, lakini ongezeko la magenge ya wafanya magendo ya binaadamu na usafirishaji wahajiri haramu kuelekea Ulaya, limegeuka kuwa tatizo kubwa, ambapo hadi sasa akthari ya wahajiri hao wamepoteza maisha yao katika mazingira ya kutatanisha. Hivi sasa kwa kuzingatia kuwa Ufaransa na baadhi ya nchi za Ulaya zinatambaliwa na moto ziliojiwashia zenyewe, kwa kutumia nara ya ubinaadamu na utoaji misaada, zinakusudia kusaini makubaliano yenye lengo la kuhitimisha wimbi hilo. Sambamba na nchi hizo kuendeleza kwa nyuma ya pazia siasa zao kwa lengo la kujisafisha na makosa yao ya huko nyuma, zinalinda pia nafasi zao katika eneo. Ahadi za fedha na misaada kemkem katika uwanja huo, zinafanyika katika fremu hiyo. Hata hivyo harakati za aina hiyo zinafeli na kugonga mwamba. Na sababu ni kwamba, kwa upande mmoja nchi kama vile Niger, inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa kutokana na harakati za kigaidi za wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram na hivyo haiwezi kuwa mshirika wa kivitendo wa ushirikiano kama huo. Na kwa upande mwengine baada ya muda kupita, nia halisi ya hatua za aina hiyo zinazochukuliwa na nchi za Magharibi huwa zinafichuka na kuzidi kudhihirika.