Idadi ya waliofariki dunia katika maporomoko ya taka Ethiopia yafikia 113
Nchini Ethiopia, idadi ya vifo vilivyosababiswa na maporomoko ya taka katika eneo la kutupa taka viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa imefikia 113
Serikali ya Ethiopia jana pia ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia maafa hayo ambayo yameitikisa nchi hiyo ambayo mji wake huo ni makao makuu ya Umoja wa Afrika AU.
Idara ya Habari ya serikali imesema waokoaji wamepata miili 41 zaidi kwenye eneo la tukio na kufanya idadi ya jumla ya vifo kufikia 113, wengi wao wakiwa ni wanawake. Maafisa wa seriakli wanasema huenda idadi hiyo ikaongezeka kwani watu 80 hawajulikano waliko baada ya maafa hayo.
Mkasa huo ulitokea baada ya makumi ya watu kufukiwa na maporomoko ya udongo katika eneo kubwa la kutupa taka, viungani mwa mji mkuu Addis Ababa Jumamosi iliyopita.

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema serikali ya Ethiopia inabeba dhima ya vifo vya makumi ya watu katika mkasa wa maporomoko ya udongo katika eneo la kutupa taka viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa.
Muthoni Wanyeki, Mkurugenzi wa Amnesty International eneo la Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu amesema kuwa, serikali ya Ethiopia inapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuzuia mkasa huo ambao ungeweza kuzuilika.