Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika aitembelea Somalia
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameongoza ujumbe wa ngazi za juu wa umoja huo katika ziara ya kuitembelea Somalia.
Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle mjini Mogadishu jana Jumamosi, Mahamat alilakiwa na Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Kheyre kabla ya kwenda katika Ikulu ya Rais na kufanya mazungumzo na Rais Mohamed Abdullahi Farmajo.
Duru za habari zinasema kuwa, mazungumzo ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Rais wa Somalia yamejikita zaidi katika masuala ya ukame na baa la njaa linaloikabili nchi hiyo ya Afrika.
Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Mahamat ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad alishinda nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika yenye makao yake mjini Addis Ababa, Ethiopia; ambapo katika ilani zake, aliahidi kuangazia zaidi masuala ya usalama na maendeleo.
Safari ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU nchini Somalia inafanyika chini ya wiki mbili baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuitembelea nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Machi 7, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN alifanya safari ya dharura katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, katika hali ambayo nchi hiyo inaendelea kusumbuliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na uhaba wa chakula na ukosefu wa usalama. Alisema, mapigano, ukame, mabadiliko ya hali ya hewa na ugonjwa wa kipindupindu ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo ikabiliwe na mazingira yasiyoweza kutasawarika.