Polisi 40 wauawa kwa kukatwa vichwa Congo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26852-polisi_40_wauawa_kwa_kukatwa_vichwa_congo_dr
Ripoti kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimesema kuwa wanamgambo wa eneo la katikati mwa nchi hiyo wamewakata vichwa maafisa karibu 40 wa jeshi la polisi ya nchi hiyo katika maeneo ya msituni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2017 12:05 UTC
  • Polisi 40 wauawa kwa kukatwa vichwa Congo DR

Ripoti kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimesema kuwa wanamgambo wa eneo la katikati mwa nchi hiyo wamewakata vichwa maafisa karibu 40 wa jeshi la polisi ya nchi hiyo katika maeneo ya msituni.

Hayo yamesemwa leo na maafisa wa eneo hilo wakisisitiza kuwa, hayo ni mauaji makubwa zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya mafisa wa polisi tangu machafuko yaibuke tena mashariki mwa Congo mwezi Agosti mwaka jana.

Msemaji wa Baraza la mkoa wa Kasai, Francois Kalamba amesema kuwa wanamgambo wa kundi la Kamuina Nsapu walishambulia polisi wa eneo hilo Ijumaa ya jana wakati walipokuwa njiani kutoka Tshikapa wakielekea Kananga na kupora silaha na magari yao. 

Jeshi la Congo linakabiliwa na kibarua kigumu kudhibiti makundi ya waasi

Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekumbwa na ghasia na machafuko makubwa na mwezi Februari mwaka huu maafisa wa serikali katika eneo hilo walisema kuwa watu zaidi ya 150 wameuawa katika mapigano yaliyotokea kwenye mkoa wa Tanganyika pekee.

Vilevile Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inawajibika kufanya uchunguzi wa ripoti za kuaminika kuhusu jinai zilizofanywa nchini humo yakiwemo mauaji ya raia yaliyofanywa na jeshi la serikali.