IGAD yaafiki kusaidia kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Somalia
Shirika la Kiserikali la Ustawi wa nchi za Mashariki mwa Afrika IGAD limeafiki kusaidia kuwarejesha kwa hiari katika nchi yao wakimbizi wa Somalia.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kumailizika mkutano maalumu wa viongozi wa nchi wanachama wa IGAD chini ya uenyeji wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya mjini Nairobi, viongozi wa IGAD wameafikiana pia kuhusu kuimarisha usalama na utulivu nchini Somalia. Aidha wametaka uwezo wa Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kulinda Amani Somalia AMISOM uimarishwe ili kurejesha usalama katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Halikadhalika viongozi wa IGAD wametaka nchi za eneo hilo zisaidiwe katika kuwalinda na kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia sambamba na kuhakikisha wanaishi katika maisha ya kibinadmau wakiwa kambini.
Mkutano huo wa Nairobi ambao ulifanyika chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn umehudhuriwa pia na marais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Ismaïl Omar Guelleh wa Djibouti na Makamu wa Rais wa Sudan, Hassabo Mohamed Abdulrahman.
Zaidi ya Wasomali milioni mbili wametawanyika huku na huku duniani kutokana na moja na migogoro ya muda mrefu sana ulimwenguni na wengi wamepata hifadhi katika nchi jirani za Kenya, Ethiopia, Yemen, Uganda na Djibouti.