Amnesty yataka kikosi cha MONUSCO Kongo DR kiongezewe majukumu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26986-amnesty_yataka_kikosi_cha_monusco_kongo_dr_kiongezewe_majukumu
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukiongezea majukumu Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2017 22:26 UTC
  • Amnesty yataka kikosi cha MONUSCO Kongo DR kiongezewe majukumu

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukiongezea majukumu Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO).

Taarifa ya Amnesty International imelitaka Baraza la Usalama kuhakikisha kuwa, kikosi cha MONUSCO kinapatiwa mahitaji yake yote ili kuhakikisha kuwa kinawadhaminia usalama raia wa nchi hiyo na kinazima wimbi la ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo linatazamiwa kupasisha azimio la kuongezewa muda wa kuhudumu kikosi cha (MONUSCO) kwa mwaka mmoja zaidi.

Wakati huohuo, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imetoa wito wa kuongezwa idadi ya askari polisi wa UN katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika. Kwa sasa kuna maafisa wa polisi 1,090 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanajeshi wa MONUSCO DRC

Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kinatazamiwa kuongezewa muda wa kuhudumu DRC katika hali ambayo, utendaji wa askari hao umekuwa ukikosolewa na wananchi na baadhi ya asasi za kiraia.

Licha ya uwepo wa MONUSCO, eneo la mashariki mwa Kongo DR limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda. Aidha itakumbukwa kuwa, askari mmoja wa MONUSCO aliuawa na wengine 31 kujeruhiwa katika shambulio la guruneti katika eneo la Kyeshero lililoko magharibi mwa mji wa Goma mashariki mwa nchi, mnamo Novemba mwaka jana 2016.