Wahajiri wengine 146 wahofiwa kufa maji wakielekea Ulaya
Makumi ya wahajiri wanaaminika kuwa wamepoteza maisha baada ya boti yao kuzama katika bahari ya Mediterania.
Mmoja wa wahajiri aliyenusurika katika ajali hiyo, raia wa Gambia ameuambia Umoja wa Mataifa kuwa, boti hiyo iliyozama ilikuwa imebeba watu 150, wakiwemo watoto wadogo na wanawake wajawazito.
Mhajiri huyo wa Gambia ameliambia Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA kuwa, boti hiyo ilitokea mji wa Sabratha, magharibi mwa Libya Jumatatu iliyopita. Ameongeza kuwa, aghlabu ya wahajiri hao ni raia wa Gambia, Mali na Nigeria.
Hayo yamejiri siku tatu baada ya mitumbwi miwili iliyokuwa na wahajiri 250 kugunduliwa na boti ya uokozi katika pwani ya Libya. Mapema mwezi huu wa Machi wahajiri wengine 25 walikufa maji baada ya boti yao kuzama katika bahari ya Mediterania, wakijaribu kueleka nchini Italia.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, wahajiri 590 wameshapoteza maisha tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 wakati wakijaribu kukimbilia barani Ulaya kupitia Libya.
Shirika la Uhamiaji Duniani IOM mapema mwaka huu lilitangaza kuwa, zaidi ya wahajiri 5,000 walifariki dunia katika Bahari ya Mediterania mwaka uliopita wa 2016 katika jitihada za kuingia kimagendo barani Ulaya.