Ethiopia yarefusha muda wa sheria ya hali ya hatari kwa miezi 4
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27064-ethiopia_yarefusha_muda_wa_sheria_ya_hali_ya_hatari_kwa_miezi_4
Bunge la Ethiopia limetangaza habari ya kurefushwa sheria ya hali ya hatari nchini humo kwa muda wa miezi minne zaidi, wiki mbili baada ya serikali kufuta sheria hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 30, 2017 11:15 UTC
  • Ethiopia yarefusha muda wa sheria ya hali ya hatari kwa miezi 4

Bunge la Ethiopia limetangaza habari ya kurefushwa sheria ya hali ya hatari nchini humo kwa muda wa miezi minne zaidi, wiki mbili baada ya serikali kufuta sheria hiyo.

Bunge hilo limepasisha kwa kishindo leo Alkhamisi sheria hiyo ambayo ilipasishwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegn miezi sita iliyopita.

Siraj Fegessa, Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, kurefushwa muda wa sheria ya hali ya hatari nchini ni kwa maslahi ya amani na usalama wa taifa hilo.

Zaidi ya watu elfu 11 wamekamatwa nchini Ethiopia tangu Oktoba mwaka jana, kwa kukiuka sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa mapema mwezi huo, kufuatia mivutano ya kisiasa na malalamiko ya upinzani wa wananchi yaliyoshuhudiwa katika miji kadhaa nchini humo miezi kadhaa kabla ya hapo.

Raia wa Ethiopia wakikabiliana na askari wa nchi hiyo

Hata hivyo kufuatia mashinikizo na makelele ya ndani na nje ya nchi, serikali ya Ethiopia iliwaachia huru takriban watu elfu 10 waliokamatwa chini ya anga ya hali ya hatari Disemba mwaka jana.

Makabila mawili ya Oromo na Amhara ambayo yanaunda karibu asilimia 60 ya watu wote wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika yamekuwa yakiituhumu serikali ya Addis Ababa kwamba inatenga na kuyanyanyasa makabila hayo kwa maslahi ya wenzao Watigray ambao wamepewa nyadhifa muhimu serikalini, jeshini na kwenye vyombo vingine vya usalama.