Mufti wa Misri: Fatwa 3000 zimetolewa kupinga kuishi pamoja Waislamu na Wakristo
Mufti wa Misri amesema kuwa asilimia 90 ya hukumu na fatwa za watu wanaofurutu ada zinawachochea watu kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuzusha mifarakano baina ya Waislamu na Wakristo.
Shawki Allam amesema kuwa, jumla ya fatwa 3000 zimefanyiwa uchunguzi katika kitengo cha Darul-Iftaa nchini Misri ambazo akthari yake zinashajiisha kubomoa makanisa na kupinga kuishi pamoja na kwa masikilizano Waislamu na Wakristo.
Sambamba na kuashiria tofauti za wanadamu kuwa ni suala lisiloepukika na linalotokana na matakwa ya Mwenyezi Mungu amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria, itikadi za kulazimisha, ni suala lisilokubalika. Amesema kuwa njama zote zinazofanywa kwa lengo la kuibua utengano na tofauti baina ya Waislamu na Wakristo nchini Misri, zimeishia kufeli. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, idadi kadhaa ya Wakristo waliuawa na watu wenye silaha wasiojulikana katika maeneo tofauti ya al-Arish, lililopo Sinai huko kaskazini mwa Misri.
Kufuatia mashambulizi hayo, Wakristo wengi walilazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia katika maeneo ya Waislamu kwa ajili ya usalama wao.