Jeshi la DRC lazima shambulizi la waasi wa Mai-Mai
-
Wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limefanikiwa kuzima shambulizi la waasi wa Mai-Mai katika kijiji kimoja cha mashariki mwa nchi hiyo na kuwalazimisha waasi hao kukimbia.
Duru za usalama za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamefanikiwa kuyafurusha makundi mawili ya waasi wa Mai-Mai ambao wiki iliyopita walikivamia kijiji cha Kasuho katika eneo la Lubero mkoani Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa duru za kiusalama wa DRC, shambulio la waasi hao wa Mai-Mai katika kijiji cha Kasuho limeua mtu mmoja.
Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia machafuko kwa miaka 20 sasa.
Jeshi la serikali na kikosi cha askari wa kofia buluu cha Umoja wa Mataifa wameshindwa kumaliza uasi, na kila leo makundi mapya ya waasi yanazuka kwenye eneo hilo yakiteka maeneo hasa ya mashariki na kuua raia pamoja na kupora utajiri wa maliasili wa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.
Wafuatiliaji wa mambo wanasema kuwa mgogoro usioisha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unachochewa na madola ya kigeni yanayoangalia kwa macho ya tamaa utajiri mkubwa wa maliasi wa nchi hiyo hasa kwa kuzingatia kuwa, kama waasi watasusiwa kweli kimataifa kuuziwa silaha na kununuliwa madini wanayouza nje ya nchi, uasi katika nchi hiyo utaweza kudhibitiwa kiurahisi.