Kupambana na ugaidi, lengo la kongamano la usalama barani Afrika
Viongozi wa masuala ya intelijensia na usalama kutoka nchi 30 za Kiafrika wanakutana mjini Khartoum, Sudan katika kikao cha siku tatu kwa lengo la kuchunguza mikakati ya kupambana na vitisho vipya na ongezeko la ugaidi barani humo.
Mohamed Atta Al-Mawla Abbas, mkuu wa idara ya intelijensia na usalama wa taifa nchini Sudan amehutubia kikao hicho na kusema kuwa, katika mikakati ya kukabiliana kwa dhati na vitisho vipya vinavyolikabili bara hilo, viongozi wa usalama wa Kiafrika wanatakiwa kufanya juhudi kubwa katika uwanja huo. Atta ameongeza kuwa, hii leo moja kati ya vitisho muhimu katika ngazi ya bara zima la Afrika ni kujiunga kwa wingi vijana wa nchi za bara hilo na makundi ya kigaidi hususan Daesh, al-Qaidah, ash-Shabab na Boko Haram. Ameongeza kuwa, kukosekana usimamizi mzuri wa kuzuia mwenendo huo kunaweza kuwa na madhara makubwa kwa kila nchi ya Kiafrika na hata katika jamii ya kimataifa.
Shimelis Woldesemayat, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Intelejensia na Usalama ya Umoja wa Afrika yenye makao yake mjini Abuja, Nigeria amesema kuwa, wapiganaji wa Kiafrika wanaoshirikiana na kundi la Daesh (ISIS) huko Syria na Iraq wanaweza kusafiri kirahisi katika nchi mbalimbali za Kiafrika, suala ambalo ni hatari kubwa kwa nchi zote za bara hilo.
Kuenea harakati za kigaidi katika nchi za bara la Afrika na kadhalika kujiunga makundi tofauti ya vijana na magenge ya kigaidi kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika, kwa muda mrefu si tu kwamba kumezisababishia matatizo nchi nyingi, bali limegeuka na kuwa tatizo kwa ulimwengu mzima. Akthari ya raia hususan vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kutokana na matatizo ya kiuchumi na kukosekana usalama, hujikuta wakihajiri kinyume cha sheria kupitia njia hatarishi kwenda Ulaya au kujiunga na makundi ya kigaidi baada ya kushawishiwa na makundi hayo.
Hivi sasa nchi nyingi za bara hilo zinakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei, umasikini na upungufu wa chakula kumeyafanya maisha katika nchi nyingi kuwa magumu. Aidha machafuko, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na kukosekana usalama kunakoshuhudiwa katika mataifa mengi ya eneo hilo, vimehatarisha fursa za uwekezaji katika masuala ya uchumi. Mbali na hayo ni kwamba, kukosekana miundombinu hususan umeme na barabara zinazofaa na hatari ya magonjwa ya kuambukiza kumezifanya akthari ya nchi nyingi za eneo hilo zishindwe kuvutia uwekezaji wa kigeni licha ya kuwa na fursa nyingi za kuvutia wawekezaji. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya uwekezaji wa nchi za Kimagharibi unafanyika barani Afrika barani kwa malengo ya ukoloni na kudhamini maslahi yao binafsi yao bula ya kutilia maanani maslahi ya Waafrika.
Kwa upande mwingine watawala wengi wa Kiafrika katika jitihada za kuimarisha tawala zao na kusalia zaidi madarakani, wamejielekeza upande wa kuchukua mikopo na misaada ya kigeni.
Misaada hiyo, si tu kwamba haijasaidia kutatua matatizo, bali ulipaji wake umezidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi hizo kiasi kwamba, mgogoro unaosababishwa na madeni ya kigeni kwa mataifa hayo ya Kiafrika umekuwa tatizo kubwa kwa nchi nyingi za bara hilo.
Wakati huo huo vita vya kuwania madaraka na migogoro ya kisiasa bado vinaendelea katika nchi nyingi za Kiafrika. Vita vya ndani nchini Sudan Kusini, mivutano ya kisiasa huko Burundi, ukosefu wa amani nchini Somalia, machafuko ya Nigeria na kadhalika mazingira ya kisiasa yaliyojaa migogoro huko Libya, yote haya yameyasafishia njia makundi ya kigaidi kuweza kuingia kwa wepesi katika nchi nyingi za bara hilo.
Mambo hayo ndio yanayozifanya nchi nyingi za Afrika kuhisi hatari zaidi kuchukua uamuzi wa kuimarisha ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kukabiliana na hatari hizo. Katika fremu hiyo, kuongezeka ushirikiano wa kijeshi na kiusalama katika ngazi ya kieneo, kuimarisha usalama, kuhitimisha tofauti za ndani na migogoro mingi ya kisiasa, kuikubali demokrasia na kuwapa raia fursa ya kuchagua viongozi wao kwa njia ya kupiga kura na kustawisha miundombinu kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiuchumi, yanaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la kujiunga wananchi wa mataifa ya Kiafrika na makundi ya kigaidi.