Jeshi na waasi Sudan Kusini watuhumiana kwa mauaji ya raia
Msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ametangaza habari ya kukimbilia nchini Uganda maelfu ya raia wa Sudan Kusini kufuatia kushadidi mapigano ndani ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Catherine Wainright, amesema kuwa zaidi ya watu elfu tatu wakazi wa mji wa Pajok, mashariki mwa Sudan Kusini wamekimbilia nchini Uganda katika kipindi kifupi kutokana na mapigano makali nchini humo.
Ameongeza kuwa, kufuatia hujuma hizo wapinzani wa serikali ya Sudan Kusini wamedai kuwa, Jumatatu iliyopita, askari wa serikali walishambulia mji wa Pajok na kuteketeza moto nyumba, kuwabaka wanawake na kuwanyonga raia wengi wa mji huo. Hata hivyo jeshi la Sudan Kusini sambamba na kukadhibisha madai hayo ya wapinzani limesema kuwa, askari wa serikali ndio waliolazimika kuingilia kati mjini humo kwa lengo la kutuliza ghasia baada ya kushadidi mapigano, uporaji mali za raia na mauaji yaliyofanywa na waasi hao.
Sudan Kusini, ilitumbukia katika mchafukoge mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumshutumu makamu wake wa zamani Riek Machar, kwamba alikuwa anapanga njama za kumpindua. Zaidi ya raia laki nane wa Sudan Kusini wamekimbilia nchini Uganda, tangu kulipoibuka machafuko nchini humo.