Watu watatu wa familia moja wapoteza maisha huko Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27424-watu_watatu_wa_familia_moja_wapoteza_maisha_huko_mogadishu
Watu wasiopungua watatu wa familia moja wameaga dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia nyumba yao kupigwa na kombora hii leo huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2017 09:45 UTC
  • Watu watatu wa familia moja wapoteza maisha huko Mogadishu

Watu wasiopungua watatu wa familia moja wameaga dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia nyumba yao kupigwa na kombora hii leo huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia.

Kombora hilo liliipiga nyumba iliyopo katika kitongoji cha Danwadagta karibu na kituo cha upekuzi cha Uwanja wa ndege wa Mogadishu. Hayo yameelezwa na afisa usalama kwa jina la Abdi Muhidin. Mtu mwingine aliyeshuhudiwa tukio hilo kwa jina la Awale Yasin ameeleza kuwa, mama na binti yake ni miongoni mwa raia hao waliouawa katika shambulio hilo ambao wanatoka katika familia moja. Shambulio hilo ni la pili kutokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu wiki hii, baada ya kutokea hapo juzi mlipuko wa gari lililotegwa bomu uliosababisha vifo vya watu saba. Mlipuko huo wa gari lililotegwa bomu ulitokea katika mgahawa mmoja  mjini Mogadishu.

Hadi kufikia sasa kundi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake huko Somalia halijatangaza kuhusika na shambulio lolote kati ya hayo yaliyotajwa, japokuwa kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulizi mengi ya kigaidi kama utegaji mabomu n.k.

Wanamgambo wa al Shabab wenye makao yao nchini Somalia 

Wakati huo huo Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia jana aliahidi kuanzisha vita vipya dhidi ya kundi la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kutoa siku sitini kwa kundi hilo kujisalimisha.