Afisa wa serikali Somalia auawa kwenye mlipuko wa bomu Mogadishu
Afisa wa serikali ya Somalia ameuawa katika mlipuko wa bomu la kutegwa garini huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia. Mlipuko huo umesababisha kifo cha afisa wa ngazi ya chini wa serikali ya Somalia. Hayo yameelezwa na Abdifatah Omar Halane Msemaji wa Meya wa Mogadishu.
Hadi kufikia sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, hata hivyo kundi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake huko Somalia limezidisha mashambulizi yake ya utegaji mabomu katika mji mkuu Mogadishu tangu kuanza kazi Rais mpya wa Somalia mwezi Februari mwaka huu.
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia Alhamisi iliyopita alitangaza kuanza mashambulizi mapya dhidi ya makundi ya kigaidi. Aidha aliwapatia siku 60 wanamgambo wa al Shabab kuweka chini silaha zao na kujisalimisha. Rais wa Somalia pia amefanya mabadiliko kwa wakuu wa jeshi na wa idara ya intelijinsia, polisi na kuteua meya mpya wa Mogadishu katika juhudi za kuboresha hali mbaya ya usalama katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyoathiriwa na machafuko kwa muda mrefu.