Uzalishaji mafuta wakwama tena kusini magharibi mwa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27600-uzalishaji_mafuta_wakwama_tena_kusini_magharibi_mwa_libya
Uzalishaji wa mafuta katika medani ya al Sharara ya kusini magharibi mwa Libya umekwama tena baada ya watu wenye silaha kufunga bomba moja la kusafirishia mafuta.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 10, 2017 23:16 UTC
  • Uzalishaji mafuta wakwama tena kusini magharibi mwa Libya

Uzalishaji wa mafuta katika medani ya al Sharara ya kusini magharibi mwa Libya umekwama tena baada ya watu wenye silaha kufunga bomba moja la kusafirishia mafuta.

Afisa mmoja wa serikali ya Libya amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, watu wenye silaha wamefunga bomba la mafuta lililokuwa likisafirisha mafuta ya kisima cha al Sharara hadi katika bandari na kituo cha mafuta cha al Zawiya kilichoko umbali wa kilomita 50 magharibi mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Uzalishaji mafuta katika medani ya al Sharara ulisimamishwa pia mwezi Machi mwaka huu kutokana na watu wenye silaha kufunga bomba la kusafirishia mafuta yanayozalishwa kwenye eneo hilo.

Mapigano baina ya makundi yenye silaha umekuwa msiba mkubwa nchini Libya

 

Shirika la Mafuta la Libya (NOC) linazalisha mapipa zaidi ya laki mbili kwa siku katika eneo la al Sharara, kiwango ambacho ni chini ya robo ya mapipa laki saba yanayozalishwa nchini Libya kila siku.

Baada ya kupinduliwa Kiongozi wa Libya, Muammar Ghaddafi mwaka 2011, kiwango cha uzalishaji mafuta kimepungua sana nchini humo.

Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia utulivu tangu wakati huo. Machafuko hayo na kukosekana serikali kuu yenye nguvu kumepelekea madola ya kibeberu kupora kwa wingi utajiri hasa wa mafuta wa Libya.

Vita baina ya pande mbalimbali hasimu vimekuwa vikikwamisha mara kwa mara uzalishaji mafuta nchini Libya.