Mkurupuko wa kuendesha waua watu 28 Somaliland
Makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kuharisha katika eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland huko kaskazini mwa Somalia.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu zimetangaza kuwa, mripuko huo wa kuendesha umesababisha vifo vya watu 28 katika kipindi cha siku kumi zilizopita huko Somaliland.
Abdi Razaq Ali Duran, afisa wa Hilali Nyekundu ya Somalia katika mji wa Buhdole karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia amesema mripuko huo unatishia maisha ya wananchi wa Somaliland, ambao tayari walikuwa wamedhoofishwa na ukame na baa la njaa.
Kadhalika eneo la Puntland linakabiliwa na hali kama hii, ambapo vifo 57 na kesi 1,600 za ugonjwa huo zimeripotiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Ulaya, Johan Heffinck, mwaka huu pekee kumeripotiwa kesi 18,000 za kipindupindu kote Somalia na kwamba kati ya wagonjwa 45, mgonjwa mmoja hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Mwezi uliopita, Hassan Ali Khayre, Waziri Mkuu wa Somalia alitangaza kuwa zaidi ya watu 110 wamefariki dunia nchini humo kutokana na ugonjwa wa kipindupindu ndani ya masaa 48.