UN yagundua makuburi mengine 17 ya umati nchini Kongo DR
Timu ya wachunguzi ya Umoja wa Mataifa imegundua makaburi mengine 17 ya umati katika mkoa wa Kasai, katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wiki mbili baada ya makaburi mengine kugunduliwa katika eneo hilo.
Taarifa ya umoja huo imesema idadi hiyo imepelekea jumla ya makaburi ya umati yaliyogunduliwa hadi sasa na UN kufikia 40, katika eneo ambalo lilishuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, watu 74 wakiwemo watoto 30 wameuawa na wanajeshi wa serikali katika eneo hilo wakati wa makabiliano hayo.
Msemaji wa serikali ya Kongo DR hata hivyo amekataa kulizungumzia sual hilo, alipotakiwa kutoa radiamali yake kuhusu kupatikana kwa makaburi hayo ya umati na shirika la habari la Reuters.
Hata hivyo huko nyuma serikali ilikanusha vikali kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya magenge ya waasi na kwamba makaburi hayo ya umati yalichimbwa na waasi wenyewe.
Mkoa wa Kasai umekuwa ukishuhudia machafuko tangu Septemba mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 400 wameuawa katika machafuko na mapigano kati ya askari usalama na wanamgambo wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu, aliyeuliwa na maafisa usalama.