UN: Watu milioni moja wamekuwa wakimbizi mkoa wa Kasai, Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28090-un_watu_milioni_moja_wamekuwa_wakimbizi_mkoa_wa_kasai_kongo_dr
Mapigano makali kati ya askari wa serikali ya jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo wa kundi moja la kikabila katika mkoa wa Kasai yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuyaacha makazi yao katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 21, 2017 23:14 UTC
  • UN: Watu milioni moja wamekuwa wakimbizi mkoa wa Kasai, Kongo DR

Mapigano makali kati ya askari wa serikali ya jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo wa kundi moja la kikabila katika mkoa wa Kasai yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuyaacha makazi yao katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

 Hayo yalielezwa jana Ijumaa na Umoja wa Mataifa. Mapigano hayo yalizuka katika mkoa wa Kasai baada ya askari wa jeshi la serikali ya Kongo kumuuwa Jean Pierre Mpandi aliyekuwa mkuu wa kundi moja la kikabila maarufu kwa jina Kamwina Nsapu mwezi Agosti mwaka jana ambaye alianzisha eti mapambano ya ukombozi dhidi ya Rais Joseph Kabila.

Yvon Edoumou, afisa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu (OCHA) amesema kuwa, ofisi hiyo imesajili wakimbizi wa ndani milioni 1.09 katika mkoa wa Kasai, katikati mwa Kongo kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.

Wakimbizi wa ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 

Afisa huyo wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, machafuko yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya Kongo ikiwemo mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Kusini yamewalazimisha raia wengine milioni mbili wayahame makazi yao.