Taasisi za kiraia Niger zatahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi
Jumuiya ya Wasomaji Bingwa wa Qur'ani na taasisi nyingine kadhaa zisizo za serikali nchini Niger zimetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wakimbizi walioko katika maeneo ya kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Mwandishi wa ParsToday nchini Niger ameripoti kuwa, Jumuiya ya Wasoma Bingwa wa Qur'ani na taasisi nyingine zisizo za serikali za Niger zimeashiria uhaba wa suhula na hali mbaya inayowasibu wakimbizi katika miji ya Diffa na Boso huko kusini mashariki mwa Niger na zimewahimiza wananchi kushiriki katika jitihada za kuwasaidia wakimbizi hao.
Jumuiya hizo zisizo za serikali zimetangaza kuwa, makumi ya familia za mji wa Boso zimelazimika kukimbia makazi na nyumba zao kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Kundi la Boko Haram ambalo lilianza kushambulia maeneo ya raia na vituo vya umma nchini Nigeria mwaka 2009 limepanua zaidi mashambulizi yake ya kigaidi katika nchi za Niger, Chad na Cameroon. Zaidi ya watu elfu 20 wameuawa hadi sasa katika mashambulizi ya kundi hilo.