Kashfa mpya ya ngono yakumba kikosi kikosi cha UN nchini DRC
Msemaji Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) amesema kumejiri vitendo vitano vya kashfa ya ngono miongoni mwa askari wa kikosi hicho mwaka huu wa 2017
Charles-Antoine Bambara msemaji wa MONUSCO amekiri kuwa kuna kesi tano za ukiukaji maadili miongoni mwa askari wa kulinda amani na kusema, Umoja wa Mataifa unatafakari kuhusu njia mpya za kukabiliana na kashfa za ngono miongoni mwa walinda amani wake.
Mwaka jana pia, ilibainika kuwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakiwadhalilisha kijinsia watoto wanne wanaoishi katika kambi ya wakimbizi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Waathirika hao wanne walinajisiwa kati ya mwaka 2014 na 2015, alibaini msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq.
Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA pia kimekuwa kikumbwa na kashfa za askari wake kuwadhalilisha kingono watoto. Hii ni katika hali ambayo askari wa Umoja wa Mataifa wana jukumu la kuwalinda raia katika nchi walizotumwa.
Askari wa Ulaya hasa wa Ufaransa pia wanatajwa kuhusika na vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu dhidi ya watoto wadogo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kimaisha kutokana na nchi yao kukumbwa na machafuko ya umwagaji damu mkubwa tangu mwaka 2013.