Sudan Kusini yaipiga marufuku televisheni ya 'Aljazeera' nchini humo
Ofisi ya kusimamia vyombo vya habari nchini Sudan Kusini, imezifunga ofisi za televisheni ya Al-Jazeera ya Kingereza kuendelea na shughuli zake ndani ya nchi hiyo.
Lija Aler Kuway, mkuu wa ofisi hiyo ya utangalizi wa vyombo vya habari amesema kuwa, hakuna mwakilishi yeyote wa shirika hilo la habari la Al-Jazeerah atakayeruhusiwa kurusha habari ndani ya Sudan Kusini hadi pale kutakapotolewa amri nyingine. Amesema kuwa uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kanali hiyo kutangaza habari za uongo kuhusiana na waasi na kwamba kutokana na suala hilo, hakuna raia wa nchi hiyo anayeruhusiwa kuiripotia kanali hiyo kwa muda huu.
Kadhalika mkuu huyo wa ofisi ya kusimamia vyombo vya habari nchini Sudan Kusini, amesema kuwa hatua ya timu ya kanali ya Al-Jazeera iliyoko nchini Uganda, kuingia ardhi ya Sudan Kusini na kufanya mahojiano na waasi, ilikuwa na lengo la kuchafua sura ya serikali katika kupambana na waasi hao ambao wanakabiliana moja kwa moja na serikali. Hivi karibuni Al-Jazeerah ya Kiingereza ilirusha habari ambayo iliituhumu serikali ya Juba kuwa ilihusika na shambulizi dhidi ya mji wa Kajo Keji, ulio katika mpaka wa pamoja na Uganda na ambao wakazi wake wengi ni wapinzani wa serikali. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya shambulizi hilo, askari wa serikali waliharibu makazi ya raia sambamba na kuifanya idadi kubwa ya wakazi wa mji huo kuwa wakimbizi.
Hii ni katika hali ambayo, kwa muda sasa serikali ya Juba imekuwa ikiwanyoshea kidole cha lawama waasi, kuwa ndio waliohusika na shambulizi hilo.