May 06, 2017 13:09 UTC
  • Wakimbizi wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waingia DRC

Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametangaza kuwa, idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wameingia nchini humo.

Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametangaza leo kuwa, kundi kubwa la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati limeingia nchini humo likikimbia machafuko yanayoendelea kuikumba nchi yao.

Wimbi la wakimbizi linaripotiwa kuikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati katika hali ambayo, hali ya nchi hiyo inayokabiliwa na machafuko inaripotiwa kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Wakati huo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa mashirika ya kutoa misaada ya kimataifa yamepunguza shughuli zao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kufuatia mashambulizi kadhaa dhidi ya wafanyakazi wao.

Wanachama wa moja ya makundi ya wabeba silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mashirika manne ya kimataifa yamesitisha shughuli zao katika eneo la Ouham na Madaktari wasio na mipaka MSF wamesema kuwa wanawatibu wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura pekee.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa nusu ya raia wote wa CAR hutegemea chakula na madawa ya misaada kila siku.

Ikumbukwe kuwa, mapigano ya hivi karibuni katika miji ya Bambari, Ouaka, mkoa wa katikati na Makoum, kusini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, yamesababisha mauaji makubwa na wakazi wengi wa maeneo hayo kuwa wakimbizi.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika mgogoro, mwaka 2013 baada ya kuzuka mapigano ya kikaumu yaliyopelekea kuondolewa madarakani serikali ya Rais François Bozizé.  

Tags