Vita vyawalazimisha watoto milioni mbili Sudan Kusini kukimbia makazi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28824-vita_vyawalazimisha_watoto_milioni_mbili_sudan_kusini_kukimbia_makazi_yao
Umoja wa Mataifa umetangaza leo kuwa vita na ukame vimewalazimisha watoto zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao nchini Sudan Kusini huku watu 21 wakiuawa katika shambulio la karibuni lililofanywa na watu wenye silaha wasiojulikana.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 08, 2017 10:55 UTC
  • Vita vyawalazimisha watoto milioni mbili Sudan Kusini kukimbia makazi yao

Umoja wa Mataifa umetangaza leo kuwa vita na ukame vimewalazimisha watoto zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao nchini Sudan Kusini huku watu 21 wakiuawa katika shambulio la karibuni lililofanywa na watu wenye silaha wasiojulikana.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi (UNHCR) kanda ya Afrika, Valentin Tapsoba, ameeleza kupitia taarifa na kuongeza kuwa hakuna mgogoro na hali mbaya ya wakimbizi inayomtia wasiwasi zaidi hivi sasa kama ya wakimbizi wa Sudan Kusini. Kwa mujibu wa UNHCR na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF), katika nchi hiyo yenye watu milioni 12, karibu robo tatu ya watoto hawaendi shule. Watoto zaidi ya milioni moja wamekimbilia nje ya Sudan Kusini huku wengine milioni moja wakibaki bila ya makaazi ndani ya nchi hiyo.

Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yameongeza kuwa watoto zaidi ya elfu moja wameuliwa kwenye mapigano huku idadi hiyo ikikadiriwa kuwa kubwa zaidi kutokana na kukosekana taarifa za uhakika za vifo nchini humo.

Wakimbizi wengi wa Sudan Kusini wamekimbilia nchi jirani za Uganda, Kenya, Sudan na Ethiopia, mataifa ambayo yenyewe hivi sasa yanahangaika kukidhi mahitaji ya chakula ya raia wao.

Rais Salva Kiir (kushoto) na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilianza mwaka 2013, miaka miwili tu tangu taifa hilo changa zaidi duniani kujitangazia uhuru wake baada ya kujitenga na Sudan, kufuatia hatua ya Rais Salva Kiir kumtimua aliyekuwa makamu wake Riek Machar. Mapigano yaliyozuka baada ya hapo yaliigawa nchi hiyo katika misingi ya ukabila na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo uliozusha mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi barani Afrika tangu ule wa baada ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda…/