Kenyatta: Jeshi la Kenya kubakia Somalia hadi Kenya iwe salama
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesisitiza kuwa askari wa nchi hiyo wataendelea kubakia Somalia hadi wafikie lengo la kuihakikishia Kenya usalama.
Akizungumza na waandishi habari kabla ya kuelekea London kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa Somalia, Rais Kenyatta ameongeza kuwa wanajeshi wa Kenya hawataondoka Somalia hadi pale Wasomali wenyewe watakapopata uwezo wa kujilinda.
Amongeza kuwa, Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kulinda Amani Somalia AMISOM kiko Somalia kwa ajili ya kudumisha usalama na hakiwezi kutoka nchi hiyo hadi iweze kupata amani na uwezo wa kujisimamia.
Askari wa Kenya wako Somalia pamoja na askari wa Uganda, Djibouti, Ethiopia na Burundi katika fremu ya kikosi cha AMISOM na wamefanikiwa kupunguza hujuma za kundi la kigaidi la Al Shabab lakini hawajaweza kuangamiza kundi hilo la magaidi wakufurishaji. Mkutano kuhusu Somalia utaofanyika London Ijumaa unatazamiwa kuwaleta pamoja wadau wa kimataifa, Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili ili kujaribu kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.