Watuhumiwa wa mauaji Kongo DR wahukumiwa vifungo jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29034-watuhumiwa_wa_mauaji_kongo_dr_wahukumiwa_vifungo_jela
Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya watu sita kwa kuhusika na mauaji na kushirikiana na makundi ya uhalifu, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2017 09:18 UTC
  • Watuhumiwa wa mauaji Kongo DR wahukumiwa vifungo jela

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya watu sita kwa kuhusika na mauaji na kushirikiana na makundi ya uhalifu, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo ya kijeshi katika mkoa wa Ituri, mbali na watu hao kuhusika na mauaji na vitendo vya uhalifu, pia walikuwa wanamiliki silaha kinyume cha sheria katika mji wa Mahagi, mkoani hapo, ambapo kutokana na kosa hilo watu sita wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, na mwingine mmoja kuhukumiwa kifungo vya miaka 10 jela.

Askari wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu

Mahakama hiyo ya kijeshi mkoani Ituri imesema kuwa watuhumiwa wanne waliohukumiwa kifungo cha maisha, walihusika na mauaji ya watu wanne ambao ni askari wawili na raia wengine wawili, mauaji ambayo yalitekelezwa tarehe saba April mwaka jana katika eneo la Mahagi. Aidha kwa mujibu wa mahama hiyo, mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifuatiliwa kwa tuhuma za kuhusika na faili la mauaji dhidi ya raia mmoja, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela. Kadhalika katika hukumu hiyo watuhumiwa wawili waliokuwa wanahusishwa na mauaji ya raia wawili hapo tarehe 29 April mwaka jana, nao wamehukumiwa kifungo cha maisha na mahakama hiyo.

Hivi karibuni pia ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza habari ya ongezeko la mapigano baina ya serikali na wanamgambo wa kikabila, mapigano ambayo yamewafanya watu milioni moja na laki mbili na 70 elfu kuwa wakimbizi. Katika hatua nyingine duru za habari katika tarafa ya Fizi ya mkoa wa Kivu Kusini zimeripoti kwamba wakazi wa eneo hilo wameanzisha doria kwa ajili ya kujilinda kutokana na uvamizi wa askari wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakazi wa vijiji vya tarafa hiyo wameamua kujilinda wenyewe baada ya askari wa serikali kuhusika katika vitendo vya uporaji wa mali za raia eneo hilo.

Wakazi wa eneo la Baraka, tarafa ya Fizi.

Siku chache zilizopita pia askari kadhaa waliofika katika tarafa hiyo kwa lengo la kutekeleza uporaji walikamatwa na kupigwa vibaya na vijana wanaolinda doria eneo hilo na kisha kuwafunga kamba na kuwapeleka hadi kituo chao cha polisi. Mishahara midogo au kutolipwa kabisa mishahara, kunawafanya askari wa serikali kuhusika katika vitendo vya uporaji wa mali za raia nchini humo.