Mamia wauawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mamia ya watu wameripitiwa kuuawa katika mapigano makali baina ya wanamgambo wabeba silaha na askari wa serikali yaliyoibuka kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu hadi sasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Richard Lyon Kasonga mmoja wa makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amenukuliwa akisema kuwa, katika mapigano makali yaliyojiri mkoa wa Kasaï, katikati mwa nchi hiyo kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi hadi sasa, jumla ya watu 390 ambao ni raia wa kawaida na askari wengine 124, wameuawa.
Mkoa wa Kasaï ulio katikati mwa taifa hilo umekuwa ukishuhudia mapigano na vitendo vya utumiaji mabavu tangu mwaka huu 2017 hadi leo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika, huku ikiwa na jamii ya watu milioni 72. Kuwa na utajiri mkubwa wa madini, kunatajwa kuwa chanzo cha kushadidi hali ya mchafukoge ndani ya taifa hilo la katikati mwa Afrika.
Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa taarifa ya umoja huo, kila siku maelfu ya watu wanalazimika kuyahama makazi yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda maeneo mengine yenye amani.