OIC yalaani mauaji ya Waislamu Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imelaani vikali mauaji ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo yametekelezwa na magaidi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka.
Katika taarifa, OIC imebainisha masikitiko yake kuhusu mauaji hayo yaliyojiri baina ya tarehe 12 na 13 mwezi huu wa Mei katika mji wa Bangassou ambapo Waislamu karibu 30 waliuawa. Aidha katika mauaji hayo askari wanne wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliuawa.
Katibu Mkuu wa OIC Dkt. Yousef Al Al-Othaimeen ametuma salamu zake za rambi rambi kwa familia za waliopoteza maisha katika hujuma hiyo. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani mauaji hayo, limewataka viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzisha uchunguzi mara moja dhidi ya waliotekeleza shambulio hilo, na kuitaka serikali ya Bangui kufanya uchunguzi kuhusiana na askari waliotoweka wa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa.
Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.