Umoja wa Mataifa wakosoa kunyongwa watu DRC bila kufikishwa mahakamani
Umoja wa Mataifa umekosoa ongezeko la vitendo vya kuwanyonga watu bila kuwapandisha mahakamani na ukiukaji wa haki za binaadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ofisi ya masuala ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sambamba na kuonya juu ya ongezeko la vitendo hivyo imesema kuwa, jumla ya raia 234 walinyongwa ndani ya mwezi uliopita wa Aprili pekee bila kushitakiwa ongezeko ambalo ni mara mbili zaidi ikilinganishwa na matukio kama hayo yaliyojiri mwezi Machi mwaka huu.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, raia wa kawaida ndio wahanga wakuu wa ukiukaji wa haki za binaadamu. Kadhalika imeongeza kuwa, kati ya raia 164 waliouawa mwezi huo katika mkoa wa Kasaï, katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 45 walikuwa ni watoto wadogo. Kufuatia hali hiyo Maman Sidikou mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo DR amesema kwamba, matukio ya kisiasa na kiusalama yaliyoongezeka katika miezi ya hivi karibuni nchini humo yaliambatana na ukiukaji wa haki za binaadamu, suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa.
Mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliibuka tangu kulipoahirishwa uchaguzi wa rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo la kutaka kusalia zaidi madarakani.