UN yabaini kuwepo ukiukwaji mkubwa wa haki za raia Yei, Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29356-un_yabaini_kuwepo_ukiukwaji_mkubwa_wa_haki_za_raia_yei_sudan_kusini
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaelezea matokeo ya uchunguzi wa kina kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili mwingine uliotekelezwa kwenye mji wa Yei jimbo la Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini kati ya Julai 2016 na Januari 2017.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2017 23:03 UTC
  • UN yabaini kuwepo ukiukwaji mkubwa wa haki za raia Yei, Sudan Kusini

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaelezea matokeo ya uchunguzi wa kina kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili mwingine uliotekelezwa kwenye mji wa Yei jimbo la Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini kati ya Julai 2016 na Januari 2017.

Ripoti hiyo iliyotolewa na kitengo cha haki za binadamu cha mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS) na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, inaorodhesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia na ukatili mwingine uliofanywa na pande zote katika mzozo wa Sudan Kusini kwa misingi ya kikabila au upande wanaounga mkono katika mzozo..

Hii inajumuisha mauaji ya watu 114 yaliyotekelezwa na majeshi yanaounga mkono serikali. Kiwango cha ukatili uliofanywa na upinzani hakiko bayana kutokana na kutokuwa na fursa ya kufika katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi hayo imesema.

Pia ripoti hiyo iliyotolewa Ijumaa imebaini kwamba ukiukwaji huo na ukatili unaweza kuwa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu na imeahidi uchunguzi zaidi.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Mambo mengine yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni pamoja na ushahidi wa mashambulizi ya kulenga raia, mauaji, uporaji, ubakaji, na uchomaji wa nyumba na majengo ya biasahra, hali iliyowafanywa maelfu ya watu kufungasha virago.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Hivi sasa Machar anaongoza waasi wanaotaka kuipindua serikali ya Machar.