Rais wa Sudan Kusini atangaza usitishaji vita wa upande mmoja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29432-rais_wa_sudan_kusini_atangaza_usitishaji_vita_wa_upande_mmoja
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini leo ametangaza usitishaji vita wa upande mmoja na kuahidi kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa katika nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 22, 2017 11:56 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini atangaza usitishaji vita wa upande mmoja

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini leo ametangaza usitishaji vita wa upande mmoja na kuahidi kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa katika nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Katika hotuba aliyotoa katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba, Rais Kiir amesema: "Nimemwagiza Mwendesha Mashtaka Mkuu kupitia haraka kesi za waliofanya uhalifu dhidi ya dola, wanaojulikana kama wafungwa wa kisiasa na kuhakikisha hatua za lazima zinachukuliwa kwa ajili ya kuwaachia huru".

"Aidha natangaza usitishaji vita wa upande mmoja utakaoanza rasmi leo", ameongeza kueleza kiongozi huyo.

Hata hivyo katika hotuba yake hiyo, rais wa Sudan Kusini hakugusia kama yuko tayari kufanya mazungumzo na makundi ya waasi, kubwa zaidi likiwa lile linaloongozwa na aliyekuwa makamu wake Riek Machar.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa nchi hiyo Alan Boswell, Rais Kiir alishawahi kutangaza usitishaji vita hapo kabla lakini hadi sasa hajawaachia huru wafungwa wowote wa kisiasa.

Rais Salva Kiir (kushoto) na hasimu wake mkuu wa kisiasa Riek Machar

Sudan Kusini, ambayo ilijitangaza kuwa taifa huru mwaka 2011, tangu mwezi Desemba 2013 imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Licha ya kutumwa walinda amani 12,000 wa kimataifa nchini humo makumi ya maelfu ya watu wameshauawa hadi sasa na zaidi ya wengine milioni tatu wamelazimika kuyahama makaazi yao na kuwa wakimbizi.

Vita hivyo vya ndani vinahusisha zaidi jeshi tiifu kwa Rais Salva Kiir na wapiganaji watiifu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar licha ya kuwepo makundi mengine ya waasi.../