Waziri wa zamani Kongo DR kuchunguzwa kwa kuhusishwa na machafuko ya Kasai
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29480-waziri_wa_zamani_kongo_dr_kuchunguzwa_kwa_kuhusishwa_na_machafuko_ya_kasai
Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema amefungua faili la uchunguzi dhidi ya aliyekuwa waziri wa serikali hiyo Clement Kanku kuhusiana na madai kwamba alihusika na machafuko yaliyoanzishwa na wanamgambo katika eneo la Kasai ambapo mamia ya watu waliuawa na wengine zaidi ya milioni moja kubaki bila ya makaazi.
(last modified 2026-04-28T05:09:17+00:00 )
May 23, 2017 11:27 UTC
  • Waziri wa zamani Kongo DR kuchunguzwa kwa kuhusishwa na machafuko ya Kasai

Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema amefungua faili la uchunguzi dhidi ya aliyekuwa waziri wa serikali hiyo Clement Kanku kuhusiana na madai kwamba alihusika na machafuko yaliyoanzishwa na wanamgambo katika eneo la Kasai ambapo mamia ya watu waliuawa na wengine zaidi ya milioni moja kubaki bila ya makaazi.

Flory Numbi, ametoa tamko hilo leo mbele ya waandishi wa habari mjini Kinshasa kufuatia ripoti iliyotolewa siku ya Jumamosi iliyopita na gazeti la The New York Times kwamba Zaida Catalan, mchunguzi wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa akifanya uchunguzi juu ya kadhia hiyo na kuuawa punde baada ya kuanzisha uchunguzi huo alikuwa na kumbukumbu ya mazungumzo ya simu yaliyorekodiwa aliyofanya waziri wa zamani wa Kongo DR Clement Kanku na mtu anayedhaniwa kuwa ni mwanachama wa kundi la wanamgambo.

Katika mazungumzo hayo, Kanku anasikika akiidhinisha uchomaji moto uliofanywa wakati wa machafuko yaliyoanzishwa na kundi la wanamgambo la Kamuina Nsapu na kusababisha uasi dhidi ya vikosi vya serikali katika eneo la Kasai, ambapo mamia ya watu waliuawa.

Zaida Catalan (kulia) na Michael Sharp

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali endapo baada ya uchunguzi huo ataridhika na ushahidi uliopo dhidi ya Clement Kanku, waziri huyo wa zamani atafunguliwa mashtaka ya kushiriki katika harakati ya uasi, mauaji, uchomaji moto wa makusudi na kushirikiana na wahalifu.

Zaida Catalan, mchunguzi wa Umoja wa Mataifa ambaye ni raia wa Sweden na mwenzake Michael Sharp raia wa Marekani waliokuwa wakifanya uchunguzi juu ya vitendo vya uhalifu vilivyofanywa katika eneo la Kasai, waliuawa mwezi Machi mwaka huu na maiti zao kugunduliwa mwezi huohuo kwenye shimo moja la kina kifupi…/