Serikali ya umoja wa kitaifa yaanza kazi Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2974-serikali_ya_umoja_wa_kitaifa_yaanza_kazi_libya
Serikali ya umoja wa kitaifa imeanza kazi nchini Libya baada ya kupasishwa na idadi kubwa ya wabunge wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2016 09:57 UTC
  • Serikali ya umoja wa kitaifa yaanza kazi Libya

Serikali ya umoja wa kitaifa imeanza kazi nchini Libya baada ya kupasishwa na idadi kubwa ya wabunge wa nchi hiyo.

Baraza la Uongozi la Libya linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilitangaza habari ya kuanza kazi serikali mpya ya umoja wa kitaifa jana Jumamosi. Baraza hilo lenye wanachama 9 lilipewa jukumu la kuunda serikali ya mapatano ya kitaifa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa Disemba mwaka jana ili kuhitimisha machafuko ya ndani nchini Libya.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunga mkono baraza hilo wiki moja baada ya makundi hasimu ya nchi hiyo kufikia makubaliano ya kisiasa tarehe 23 Disemba. kwa msingi huo serikali ya umoja wa kitaifa ilipaswa kuundwa nchini Libya katika kipindi cha siku 30. Hata hivyo jambo hilo lilicheleweshwa, suala ambalo lilizidisha mashinikizo ya kisiasa ya nchi za Kiarabu na Kiafrika dhidi ya Baraza la Uongozi la Libya.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mashinikizo hayo ya kisiasa yalitokana na wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuhusu uwezekano wa kusonga mbele zaidi kundi la kigaidi la Daesh nchini Libya. Kwani kucheleweshwa hatua ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kunaweza kuwa miongoni mwa sababu za kueneza zaidi machafuko na ushawishi wa kundi la kigaidi la Daesh. Kwa msingi huo wachambuzi hao wanasema, kuundwa kwa serikali hiyo ni jambo la dharura kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi hususan Daesh nchini Libya.

Wanachama wa Baraza la Uongozi la Libya wameitaka jamii ya kimataifa kushirikiana tu na serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Ikumbukwe kuwa Libya imekuwa ikitawaliwa na serikali mbili tofauti.

Wabunge mia moja kati ya 198 wa Bunge la Libya wametoa taarifa wakitangaza uungaji mkono wao kwa serikali ya maridhiano ya kitaifa yenye wanachama 18. Kwa msingi huo Baraza la Uongozi la Libya limetangaza kuwa taarifa ya wabunge mia moja ni sawa na king'ora cha kuanza kazi serikali ya umoja wa kitaifa.

Pamoja na hayo yote hadi sasa bado haijajulikana serikali hiyo ya umoja wa kitaifa nchini Libya itafanya vipi kazi zake. Baraza la Uongozi la Libya limeitaka jamii ya kimataifa na taasisi za kieneo na kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kusitisha kabisa aina zote za ushirikiano na kundi au taasisi yoyote isiyokuwa chini ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.

Serikali mbili tofauti za Libya ikiwa ni ile yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo inayotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa na ile ya Tripoti ambayo inadhibiti maeneo la magharibi mwa Libya na haitambuliwi rasmi kimataifa zinapinga suala la kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo makubaliano hayo yanaungwa mkono na nchi muhimu duniani. Pamoja na hayo nchi kubwa hadi sasa hazijatangaza misimamo yao kuhusu tangazo la Baraza la Uongozi la Libya la kuanza kazi rasmi serikali ya umoja wa kitaifa.