Maandamano Morocco kupinga polisi kumsaka mwanaharakati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29742-maandamano_morocco_kupinga_polisi_kumsaka_mwanaharakati
Mamia ya watu wameandamana katika mji wa al-Hoceima kaskazini mwa Morocco kupinga hatua ya polisi kumsaka mwanaharakati na kutiwa mbaroni waandamanaji 20 siku chache zilizopita.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
May 29, 2017 03:01 UTC
  • Maandamano Morocco kupinga polisi kumsaka mwanaharakati

Mamia ya watu wameandamana katika mji wa al-Hoceima kaskazini mwa Morocco kupinga hatua ya polisi kumsaka mwanaharakati na kutiwa mbaroni waandamanaji 20 siku chache zilizopita.

Waandamanaji wakiwa wamebeba mabango na wakipiga nara dhidi ya serikali waliandamana Jumapili jioni kutangaza uungaji mkono wao kwa Nasser Zefzafi ambaye polisi imetoa waranti ya kukamatwa kwake.

Polisi walitoa waranti hiyo Ijumaa baada ya Zefzafi kumpinga khatibu wa sala ya Ijumaa ambaye katika hotuba yake alikosoa maandamano ya kupinga ufisadi. Baada ya tukio hilo maafisa wa polisi walianza kumsaka Zefzafi  wakisema atafunguliwa mashtaka ya kuvuruga hotuba msikitini. Hatua hiyo ya polisi ilipelekea kuibuka machafuko baina ya polisi na wafuasi wa Zefzafi. Mwanaharaakti huyo ametuma ujumbe katika mitandao ya kijamii na kusema yuko salama na hajakamatwa.

Kufuatia tulio hilo maandamano makubwa yameripotiwa kote Morocco kuwaunga mkono waandamanaji wa al Hoceima. Maandamano yaliripotiwa Jumapili katika miji ya Casablanca, Beni, Tangier, Nador, Imzouren, na karibu na jengo la bunge katika mji mkuu Rabat.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji Morocco

Maandamano ya kupinga ufisadi yamekuwa yakifanyika nchini Morocco tokea mwaka jana wakati mchuuzi wa samaki alipokanyagwa na lori la kubeba taka wakati akijaribu kuchukua samaki wake waliokuwa wamechukuliwa na maafisa wa polisi kwa sababu alikuwa akiuza bidhaa sehemu isiyotakiwa.

Mwanaharakati wa Moroccco, Miriyam Aouragh anasema maandamano ya al Hoceima ni muendelezo wa mwamko wa watu wa Morocco ulioanza sambamaba na mwamako wa watu wa Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati mwaka 2001 na kupelekea madikteta kadhaa kuangushwa.

Kuna umasikini mkubwa ma ukosefu wa ajira Morocco, nchi ambayo imekuwa ikitawaliwa na mfumo wa ufalme kwa miaka 350 sasa.