Umoja wa Mataifa: Machafuko Sudan Kusini si ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29774-umoja_wa_mataifa_machafuko_sudan_kusini_si_ya_kibinadamu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa na kueleza kuwa, machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu katika nchi ya Sudan Kusini ni vya kidhalimu na visivyo vya kibinadamu.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 30, 2017 00:00 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Machafuko Sudan Kusini si ya kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa na kueleza kuwa, machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu katika nchi ya Sudan Kusini ni vya kidhalimu na visivyo vya kibinadamu.

Sambamba na kukemea vikali vitendo vya utumiaji mabavu huko Sudan Kusini, Antonio Guterres amesema kuwa, kunafanyika juhudi za kuongeza misaada ya kibinadamu ya umoja huo ili kuzuia kutokea mauaji ya kizazi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amezitaka nchi wanachama wa umoja huo kuwa na ushiriki zaidi katika mipango ya amani ya Sudan Kusini na kusaidia juhudi za kurejesha amani na misaada kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan Kusini. 

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa na za mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu zimekuwa zikitoa onyo juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu kutokana na hali ya nchi hiyo kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Ripoti za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinaonyesha kuwa, idadi ya wakimbizi wa Sudan Kusini imekuwa ikiongezeka kila siku.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.