Papa afuta safari ya Sudan Kusini kutokana na sababu za 'kiusalama'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29820-papa_afuta_safari_ya_sudan_kusini_kutokana_na_sababu_za_'kiusalama'
Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican yamefuta safari ya Kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis, nchini Sudan Kusini.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
May 30, 2017 23:29 UTC
  • Papa afuta safari ya Sudan Kusini kutokana na sababu za 'kiusalama'

Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican yamefuta safari ya Kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis, nchini Sudan Kusini.

Greg Burke, msemaji wa Vatican amesema safari ya Papa Francis nchini Sudan Kusini iliyotazamiwa kufanyika mwaka huu imefutwa. Hata hivyo hajatoa sababu za kufutwa kwa safari hiyo wala tarehe nyingine ya ziara hiyo katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Hata hivyo duru za kuaminika ndani ya Vatican zimefichua kuwa, safari hiyo imefutwa kutokana na sababu za kiusalama na kilojistiki. Papa alitazamiwa kufanya safari hiyo pamoja na Askofu Mkuu wa Canterbury, makao makuu ya Kanisa la Kianglikana, Justin Welby, katika juhudi za kuimarisha umoja miongoni mwa wafuasi wa makanisa hayo mawili.

Serikali ya Sudan Kusini ilikuwa imejiandaa kumpokea kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani mwezi Oktoba mwaka huu, katika safari ambayo Vatican haijawahi kutangaza rasmi kuifahamu.

Papa na Mkuu wa Azhar mjini Cairo

Sudan Kusini ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya Rais Salvaa Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake Salva Kiir kwamba alikula njama za kutaka kumpindua madarakani, mzozo ambao umesababisha maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Papa alifanya safari ya siku mbili nchini Misri, ambapo mbali na kukutana na viongozi wa serikali ya Cairo, alikutana na kufanya mazungumzo na Ahmad Tayyib, Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu nchini humo cha al-Azhar. Kadhalika alihudhuria kongamano la amani duniani ambalo lilifanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo, lililoandaliwa na Azhar.